Na Mwandishi Wetu
Wataalamu wa UNESCO wamewasili nchini mapema wiki hii kwa ajili ya uthibitishaji upya (Revalidation) wa Hifadhi ya kijiolojia ya “Ngorongoro Lengai UNESCO Global Geopark” na kutembelea maeneo mbalimbali ndani na nje ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Wakati wa ziara yao ndani na nje ya Hifadhi hiyo ujumbe huo ulitembelea eneo linalojengwa Makumbusho ya Hifadhi ya Kijiolojia ya Ngorongoro-Lengai UNESCO Global Geopark, eneo la nyayo za Laetoli, Makumbusho ya Olduvai, bonde la Olduvai, mchanga unaohama.
Vilevile wametembelea jamii za makabila ya wairaqw, wahadzabe na wadatoga yanayoishi Wilaya ya Karatu, shule za msingi za Tumaini Junior Pre and Primary School na shule ya Father Lieberman Pre and Primary School Karatu kwa ajili ya kuona shughuli za utunzaji wa mazingira, uhunzi, urithi wa utamaduni zinazofanywa na makabila na shule hizo kuona jinsi Hifadhi inavyoshirikisha jamii katika kuhifadhi urithi wa utamaduni na mazingira yanayowazunguka.
Aidha, wataalam hao ambao ni wabobezi katika eneo la utalii wa Jiolojia na akiolojia wametembelea Kreta ya Ngorongoro kuona alama mbalimbali za jiopaki pamoja na kutembelea eneo la Laetoli kuangalia tabaka mbalimbali zilizotunza historia ya kidunia kuhusu wanyama na binadamu wa kale duniani walioishi takribani miaka milioni 3.6 iliyopita na kuona jitihada za Serikali kupitia NCAA katika uhifadhi wa urithi huo.
Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Dkt. Elirehema Doriye akiwaaga wataalam hao amewahakikishia kuwa Mamlaka hiyo itaendelea kuhifadhi, kulinda, kutangaza na kufuata masharti na miongozo ya UNESCO katika kulinda hadhi ya eneo hili ili kuendelea kuwa Hifadhi ya Kijiolojia inayotambulika kama “Ngorongoro Lengai UNESCO Global Geopark” ambapo Tanzania ni nchi ya pili Afrika kuwa na hadhi hiyo baada ya nchi ya Morocco.
Maeneo yenye hadhi za Jiolojia (Geopark) za UNESCO zinakaguliwa kwa kina kila baada ya miaka minne kwa ajili ya kupima na kuona ufanisi na ubora wao kupitia shughuli mbalimbali zinazofanyika katika maeneo hayo kwa kufuata vigezo vilivyoainishwa na UNESCO.